Visawe |
---|
Maswali kadirifu |
- Haya ni maneno yaliyo na maana sawa au yanayokaribiana sana kimaana | kwa maana.
1. Mtu – mja, adinasi, mahuluku, insi, binadamu.
Mtu [a-wa]: kiumbe anayetembea wima ambaye hutumia fikira zake kwa ustadi bainifu zaidi ya viumbe vyote.
Mfano katika sentensi - Mtu huyo ni mwoga | watu hawa ni waoga.
2. Rafiki – msena, mwandani, bui, muhibu, sahibu, somo, msiri, mwenzi.
Rafiki [i-zi]: mtu anayeaminiana na kupendana namwingine.
Mfano katika sentensi :-
a) Nilikula kwenye kafeteria na sahibu wangu.
b) Nyaiko na Nyambane ni rafiki. Kila mara, wao hupatikana pamoja.
3. Adui – hasimu.
Adui [a-wa]: mtu au kiumbe anayemfanyia mtu mwingine uovu.
Mfano katika sentensi: Paka na panya walifanyika hasimu.
4. Baba – abu
Baba [a-wa]: mzazi wa kiume.
Mfano katika sentensi - Leo tulikutana na baba wa taifa (rais) kwenye ikulu.
5 Mama – nina
Mama [a-wa]: mzazi wa kike.
Mfano katika sentensi:-
a) Mama yangu anapenda ukulima zaidi.
b) Kitinda mimba wetu anafanana na Mama.
6. Msichana – banati, gashi, binti, mwanamwali.
Msichana [a-wa]: Kijana wa kike aliyebaleghe lakini bado hajaolewa au kuzaa.
Mfano katika sentensi: Msichana huyu anasomea uhandisi katika chuo kikuu cha Egerton.
7. Mvulana – mvuli, ghulamu
Mvulana [a-wa]: Kijana wa kiume aliyebaleghe na ambaye hajafikia umri wa miaka kama thelathini na tano hivi.
Mfano katika sentensi: Kijana huyo anafanya vibaya, hatii wazaai wake. Amesahau kuwa asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu.
8. Soko – chete, gulio.
Soko [li-ya]: mahali penye mkusanyiko wa wauzaji na wanunuzi wengi wa bidhaa za rejareja.
Mfano katika sentensi: Binti na Shaja wametumwa gulioni.
9. Nyumbani – kiamboni, mastakimuni, chengoni
Nyumbani [ki]: mahali mtu anakoishi.
Mfano katika sentensi: Nyumbani kwao kuna matunda mengi sana.
10. Hasira – mafutu, kero, hamaki, ghadhabu.
Hasira [i-zi]: Ghadhabu.
Mfano katika sentensi: Baba alishikwa na hasira alipoona ngo'mbe wanaharibu mahindi shambani.
11. Lengo – dhamira, nia, azma, kusudi, gharadhi, tarajio, tumaini, matilaba.
Lengo [li-ya]: Kitu au jambo analotazamia mtu.
Mfano katika sentensi: Lengo la Salasha kuu la kwenda gulioni lilikuwa ni kununua mbaazi.
12. Tajiri – mkwasi, mlalaheri
Tajiri [a-wa]: Aliye aliye na mali nyingi.
Mfano katika sentensi: Tajiri huyo alipoaga, aliwacha pesa taslimu bilioni mia saba kwenye benki.
13. Maskini – mlalahoi, fukara, hawinde, mkata, fakiri.
Maskini [a-wa]: Mtu asiyekuwa na pato la kutosha.
Mfano katika sentensi: Rais alitoa fedha taslimu bilioni kumi kujenga miradi ya kupea maskini mapato katika nchi yetu.
14. Pesa – njenje, ngwenje, fedha, hela
Pesa [i-zi]: Sarafu au noti zenye dhamani zilizoidhinishwa rasmi kutumika katika ununuzi na uuzaji.
Mfano katika sentensi: Sina hela hata moja kwenye benki.
15. Uzembe – uvivu, ajizi.
Uzembe [u]: Hali ya kufanya mambo bila ya makini.
Mfano katika sentensi: Kila wakati wanafunzi wazembe hawapiti mtihani.
16. Maringo – madaha, madaha
Maringo [-ya]: Mwenendo au tabia ya kujivuna.
Mfano katika sentensi: Nilimwona Bi. Harusi akitembea kwa madaha.
17. Uso – wajihi
Uso [u-zi]: Sehemu ya mbele ya kichwa kuanzia kwenye paji hadi kidevuni.
Mfano katika sentensi: Niamkapo asubuhi, mimi huosha uso wangu.
18. Mke – ahali.
Mke [a-wa]: mwanamke aliyeolewa.
Mfano katika sentensi: Mke wa Ngaira ni mpishi hodari.
19. Familia – aila, mlango
Familia [i-zi]: Baba, mama, na wana.
Mfano katika sentensi: Tunapenda wageni katika familia yetu.
20. Barabara – tariki, gurufa, baraste.
Barabara [i-zi]: Njia pana ya magari.
Mfano katika sentensi: Barabara kuu ya kwenda Thika imejaa mlolongo wa magari.
21. Ugonjwa – maradhi, ndwele.
Ugonjwa [u-ya]: Kitu kinachosababisha mtu, mmea, au mnyama kuwa na afya mbaya.
Mfano katika sentensi: Nyanya amepona ugonjwa wa kifua kikuu.
22. Hongo – rushwa, chai, chirimiri, chauchau, kadhongo, chichiri, mvugulio.
Hongo [i-zi]: Malipo au zawadi anayotoa mtu ili kupata haki.
Mfano katika sentensi: Watu wengi walipoteza kazi katika nchi ya Tanzania kwa sababu ya kukubali hongo.
23. Mwizi – luja, mkupuzi, pwagu, pwaguzi
Mwizi [a-wa]: Mtu mwenye tabia ya kuchukua kisicho chake bila ruhusa.
Wezi watatu walishikwa na polisi mafichoni mwao kando ya mto Zambezi.
24. Jela – gereza, husuni
Jela [i-zi]: Pahali wanapowekwa wahalifu wa sheria, waadhibiwe ili wajirekebishe.
Mfano katika sentensi: Mati alishangaa kuwaona kina mama gerezani.
25. Afya – siha, udole
Afya [i-zi]: Hali nzuri ya mwili, bila ya magonjwa.
Mfano katika sentensi: Mimea hiyo ina afya nzuri.
26. Jitimai - huzuni, kihoro, simanzi.
Jitimai [-i]: Hali ya kuwa na masikitiko au majonzi.
27. Fujo – ghasia, zogo, zahama
Fujo [i-zi]: Hali ya kutokuwako utulivu.
Mfano katika sentensi: Fujo ilizuka wakati wanariadha hawa walipotangazwa washindi.
28. Ukuta – kiambaza
Ukuta [u-zi]: Sehemu ya nyumba kutoka chini iliyosimama wima.
Mfano katika sentensi: Ukuta ule una nyufa.
29. Usingizi – ndezi, gonezi,
Usingizi [-u]: Hali ya kupumzika kwa mwili na akili wakati wa kulala.
Mfano katika sentensi: Niliota nikiwa usingizini.
30. Kazi – amali, gange
Kazi [i-zi]: shughuli anayofanya mtu.
Mfano katika sentensi: Kazi yake ni kutumwa ofisini.
31. Mavazi – lebasi
Mavazi [li-ya]: kitu kama vile nguo, au ngozi, kinachovaliwa mwilini.
Mfano katika sentensi: Wana hawa watavaa mavazi meupe.
32. Mtoto – mkembe
Mtoto [a-wa]: Mwana mchanga
Mfano katika sentensi: Mtoto huyu ana vidonda kwenye miguu yake.
33. Makamu – naibu
Makamu [a-wa]: Mtu wa pili katika cheo.
Mfano katika sentensi: Makamu wa rais ana kesi kortini.
34. Kitanda - Samadari
Kitanda [ki-vi]: kifaa cha nyumbani chenye umbo wa mstatili na miguu minne, kinachotumiwa kwa kulalia.
Mfano katika sentensi: Kitanda ulichokilialia hujui kunguni wake.
35. Moyo – mtima, fuadi.
Moyo [u-i]: kiungo cha mwili kilichoko kwenye sehemu ya kifua kati ya mapafu, ambacho husukuma damu ili ienee mwilini kwa kupitia kwenye mishipa.
Mfano katika sentensi: Babu alipatikana na ugonjwa wa msukumo wa damu.
36. Kijiji – kitongoji, kaya, karia.
Kijiji [ki-vi]: mahali panapoishi watu wengi pamoja ambapo si mji.
Mfano katika sentensi: Kwetu kiamboni kumejaa nyani.
37. Fanicha – samani
Fanicha [i-zi]: vyombo vya nyumbani kama vile meza, viti, vitanda, na kabati.
Mfano katika sentensi: Mama yangu anatengenezewa fanicha zake kwenye karakana ya Bwana Mcheshi.
38. Ndoa – nikahi, nikaha, arusi.
Ndoa [i-zi]: Makubaliano rasmi ya mwanamume na mwanamke kuishi pamoja kama mume na mke.
Mfano katika sentensi: Bwana na Bi. Martin wanatia sahihi cheti chao cha ndoa.
39. Ndoto – ruiya, njozi.
Ndoto [i-zi]: maono yatokeayo usingizini.
Mfano katika sentensi: Maina aliota ndoto kwamba amesafiri na malaika.
40. Soka - kandanda, gozi, kabumbu.
Soka [i-zi]: mchezo wa mpira wa miguu.
Mfano katika sentensi: Kijana huyu anapenda sana kucheza soka.
41. Furaha – faraja, bashasha, naima, ucheshi
Furaha [i]: Hali ya uchangamfu, au ukunjufu wa moyo. Pia yaweza kumaanisha hali ya kuridhika.
Mfano katika sentensi: Nilijawa bashasha, nilipomwona mwanangu aliyepotea amerejea mastakimuni.