Matumizi ya 'ki'
Silabi ki- ina matumizi mbalimbali kulingana na muundo wa sentensi.
'ki' ya wakati inatumika katika:
i) Wakati uliopita hali ya kuendelea k.m. Walikuwa wakiimba kwa furaha.
ii) Wakati ujao hali ya kuendelea k.m. Watakuwa wakiimba kwa furaha.
iii) Wakati timilifu hali ya kuendelea k.m Wamekuwa wakiimba kwa furaha.
Muhimu
Ni makosa kutumia na badala ya ki k.m.
1. Walikuwa wanaimba kwa furaha. X
2. Watakuwa wanaimba kwa furaha. X
3. Wamekuwa wanaimba kwa furaha. X
Ki- ya masharti hutumika kuonyesha kuwa ni lazima kitendo fulani kitekelezwe ili pawe na matokeo fulani.
k.m. Ukisoma kwa bidii, utafua dafu. MAANA YAKE: Lazima/sharti usome kwa bidii ili ufue dafu.
Ukanushaji wa ki-ya masharti huwa ni -sipo- k.m. Mkitufikia tutamsaidia. Msipotufikia hatutamsaidia.
Ki- hii hutumika kudunisha nomino ili iwe katika hali ya udogo.
Nomino zote katika hali ya udogo katika umoja huchukua kiambishi ki k.m. mtoto – kitoto, njia – kijia.
Kiambishi ki- hutumika katika viarifu vya ngeli ya KI-VI hali ya umoja k.m. Kitabu asomacho kinapendeza.
Ki- hii huwekwa mwanzoni mwa baadhi ya nomino na kuzifanya ziwe vielezi.
Inatumika badala ya kifananisho kama k.m. Anafanya mambo kama mtoto -Anafanya mambo kitoto.
Ki- hii hutumika kuwakilisha nomino katika ngeli ya KI-VI hali ya umoja k.m. Anakibeba kikapu; Chakula ki mezani.